Browse results

Ikisiri

Makala hii inalenga kufafanua dhima za kipragmatiki zinazodokezwa kwa kiunganishi ‘na’ baina ya vishazi ambatani katika lugha ya Kiswahili. Dhima hizo huonyesha mahusiano yaliyopo baina ya vishazi vilivyoambatanishwa kwa kiunganishi hicho. Makala hii inaongozwa na nadharia ya Uhusiano ya Sperber na Wilson ambayo inahusu utambuzi wa binadamu na mawasiliano. Data zilizotumika katika makala hii zimepatikana katika machapisho ya kifasihi, hotuba na magazeti. Makala imeonyesha kuwa kiunganishi ‘na’ kina dhima mbalimbali za kipragmatiki ambazo ni uongezi, usababishi, ukinzani, usambamba na ufafanuzi. Dhima hizo ni fasiri ya mahusiano yaliyopo baina ya vishazi ambatani ambayo hayakusemwa kwa uwazi. Makala imeonyesha kuwa kiunganishi ‘na’ ni kiashiria muhimu cha kiisimu kinachomwongoza mshiriki wa mazungumzo kupata fasiri iliyokusudiwa kwa kudhibiti mchakato wa ufahamu. Pia, makala imeonyesha kwamba kiunganishi ‘na’ hutumika sambamba na viashiria vingine vya kiisimu na vya kiulimwengu kuashiria fasiri mahususi iliyokusudiwa baina ya vishazi vilivyoambatanishwa.

Full Access
In: Utafiti
Author:

Ikisiri

Kisa kinachoelezwa katika simulizi ya Edipode katika tamthilia ya Mfalme Edipode (Sofokile, 1971) kinafanana kwa karibu sana na kisa kinachosimuliwa katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi (Mulokozi, 1998). Sababu kubwa zilizochangia kufanana kwa simulizi hizi mbili zinaweza kuelezwa kwa kuzingatia misingi ya kinadharia, hususan Nadharia ya Mageuko na Nadharia ya Msambao. Wakati Nadharia ya Mageuko ikidai kuwa simulizi yoyote ile ni matokeo ya mabadiliko ya ndani ya jamii yanayochagizwa na mazingira, Nadharia ya Msambao inasisitiza kuwa simulizi huenea kutoka sehemu moja hadi nyingine; kamwe haiwezekani simulizi mbili zinazofanana kuibuka katika jamii mbili ambazo hazijawahi kukutana. Makala hii imechunguza sababu za kufanana kwa visa katika simulizi teule kwa kutumia misingi ya nadharia hizo mbili. Kwa kuzingatia hoja mbalimbali, imehitimishwa kuwa simulizi ya Nyakiiru Kibi, pamoja na kutungwa takribani karne 24 baada ya ile ya Edipode, si kiatani cha Edipode. Simulizi hii imechimbuka katika eneo la Maziwa Makuu na inaonekana ni tukio linalofungamana na historia ya jamii husika huku ikijumuisha visakale hapa na pale.

Full Access
In: Utafiti
Author:

Ikisiri

Wanahistoria na wanafasihi wameendelea kujadili uwezo wa fasihi ya Kiafrika kusawiri historia ya Afrika. Baadhi ya wataalamu wanadai kwamba fasihi ya Kiafrika haina uwezo wa kuakisi ukweli wa kihistoria; wengine wanaona kwamba ni baadhi tu ya tanzu za fasihi zinazoweza kusawiri historia ya jamii fulani. Aidha, wengine wanaona kuwa fasihi, kwa ujumla wake, bila kujali utanzu, husawiri historia ya jamii fulani. Data zilizobainishwa hapa zinaonyesha kwamba aina zote za kazi za fasihi – ushairi, tamthilia, riwaya, na fasihi simulizi – zimesawiri historia ya jamii mahususi za Kiafrika. Hivyo, kazi za fasihi ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya data za kihistoria.

In: Utafiti
Author:

Ikisiri

Uchaguzi wa mtu kuitumia lugha yake kama njia ya ukombozi huanza na uamuzi wa kifikra. Uamuzi huo wa kifikra ni hatua ya ukombozi. Ni uamuzi ambao hatimaye humpa mtumiaji wa lugha mamlaka ya kuchukua hatua zaidi za kujitegemea. Ni ukombozi wa kiisimu ambao, hatimaye humpatia mtumiaji wa lugha nguvu binafsi. Lugha ni mamlaka; na wakati mwingi mamlaka huzaa nguvu. Ingawa hapa ‘nguvu’ inamaanisha uwezo wa mtu binafsi; na ‘mamlaka’ ni dhana ya kisheria, lakini dhana hizi mbili zinahusiana katika uchambuzi huu wa kujenga uwezeshaji kupitia matumizi ya lugha. Katika kuchunguza mawazo ya Frantz Fanon kuhusu dhana ya ukombozi wa fikra kwa Waafrika kama inavyojitokeza kupitia Lugha ya Kiswahili, nadharia ya Bobby Wright ya fikraufu inatoa nafasi kuangalia namna utambulisho wa watu unavyoweza kubomolewa kupitia matumizi ya lugha isiyokuwa ya asili kwao.

In: Utafiti
Author:

Ikisiri

Usimulizi katizi ni mbinu ya Kirasimi inayotawala riwaya za Shaaban Robert. Kupitia mbinu hii mwandishi huyu humkatiza msimuliaji katika bunilizi ili aweze kutoa fundisho fulani alilokusudia. Mbinu hii ya ukatizi imesaidia nathari hizi kutengeneza ukuruba baina ya msomaji na msimuliaji na kumfanya msomaji yeyote aweze kufuatilia kwa makini msuko na mtiririko wa visa katika bunilizi za mwandishi huyu. Kusudi la makala hii ni kuchunguza dhima anuai zinazolengwa na mwandishi kupitia mbinu hii na kubainisha namna dhima hizo zinavyosawiri makusudi ya mwandishi katika kuileta karibu hadhira yake ipate kufahamu kile anachokusudia. Ili kujua hayo, mtafiti alinukuu sehemu mbalimbali za masimulizi zinaonesha mbinu hiyo ya ukatizi kutoka katika riwaya lengwa.

In: Utafiti

Ikisiri

Tafiti juu ya matumizi ya lugha katika vyombo vya habari zimethibitisha kuwapo kwa makosa kadhaa ya lugha katika utoaji wa habari. Makala haya, yanamakinikia makosa ya kisarufi katika matini andishi za habari za BBC Swahili na DW Kiswahili. Sampuli ya makala kumi kutoka kila tovuti ya chombo husika zilichanganuliwa kulingana na nadharia ya Corder (1967). Makosa ya udondoshaji, uchopekaji, upatanisho wa kisarufi, umoja na wingi, mpangilio wa vipashio na mantiki yalithibitika. Sababu za kufanyika kwa makosa hayo ni pamoja na: kutomudu sarufi ya Kiswahili, kukosa umakini katika uandishi na uhariri, athari za lugha mama, lugha za kigeni, lugha ya mazungumzo, na uteuzi mbaya wa msamiati. Vilevile, ilibainika kuwa makosa hayo yana athari hasi kwa wazungumzaji wa lugha pamoja na lugha yenyewe. Hata hiyo, tafiti zaidi zinapaswa kufanywa juu ya mazingira yachocheayo uvumilivu wa makosa ya lugha katika utangazaji wa habari kwa Kiswahili.

In: Utafiti

Ikisiri

Makala hii inachambua baadhi ya maandiko muhimu yatokanayo na mtaala kwa kutoa ufafanuzi wa kina juu ya dhana na vipengele mahususi vya maandiko hayo ambavyo mwalimu wa somo la Kiswahili hupaswa kuvizingatia katika uwasilishaji wa somo lake. Lengo la uchambuzi huu ni kuonesha athari za kutotumia vizuri maandiko hayo na umuhimu wake kwa walimu katika kufundishia somo la Kiswahili. Ufafanuzi umejumuisha maandiko ya aina tatu nayo ni muhtasari, azimio la kazi na andalio la somo. Uchambuzi huu unatokana na kuwepo kwa matumizi ya maandiko hayo isiyosahihi, walimu kutokutumia maandiko hayo kwa kigezo cha uhaba wa upatikanaji na ukosekanaji wa ufahamu wa matumizi ya maandiko hayo. Kutokana na sababu hizo na kwa kuwa lugha ya Kiswahili kimawanda asili ya matumizi yake ni Tanzania, ni muhimu kuwepo kwa andiko hili ili kumwezesha mwalimu wa somo la Kiswahili kutumia maandiko hayo kwa ufanisi na kuhimiza uandaaji wa maandiko hayo kwa idadi inayotosheleza ili kupunguza uhaba. Data za kuwezesha uandishi wa makala hii zimepatikana kwa njia ya mapitio ya maandiko na matini mbalimbali na kutafsiri rejea zilizoandikwa kwa lugha za kigeni hasa Kiingereza. Imebainika kupitia makala hii kuwa kuna athari zinazotokana na kutotumia maandiko hayo kwa walimu jambo ambalo limesababisha maandiko haya kutotumika ipasavyo.

In: Utafiti

Ikisiri

Viambishi nafsi ni miongoni mwa viambishi ambatizi ambavyo hupachikwa mwanzoni mwa vitenzi vya Kibantu (yaani kabla ya mzizi). Kazi kubwa ya viambishi nafsi ni kuleta upatanisho wa kisarufi. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa viambishi vya uambatizi hutokea kabla ya mzizi wa kitenzi, tofauti na vile vya unyambulishaji vinavyobadili kategoria au maana vinavyotokea baada ya mzizi. Makala hii inachunguza nafasi ya viambishi nafsi katika kitenzi cha Kikuria (E43). Data iliyotumika ni ya maktabani, hasa kutoka kwenye chapisho la Charwi (2017) na kutoka maandiko mengine ya Kikuria. Nadharia iliyotumika ni Nadharia ya Uambatizi kama inavyoelezwa na Stump (2001), ambayo inafafanua kuwa kila neno linaloambikwa ndani ya sentensi linabeba seti ya sifa za kimofosintaksia. Makala hii imebaini kuwa viambishi hivi vinaweza kutokea kabla au baada ya mzizi wa kitenzi na havibadili kategoria au maana ya neno.

In: Utafiti