Search Results
Ikisiri
Makala hii inalenga kufafanua dhima za kipragmatiki zinazodokezwa kwa kiunganishi ‘na’ baina ya vishazi ambatani katika lugha ya Kiswahili. Dhima hizo huonyesha mahusiano yaliyopo baina ya vishazi vilivyoambatanishwa kwa kiunganishi hicho. Makala hii inaongozwa na nadharia ya Uhusiano ya Sperber na Wilson ambayo inahusu utambuzi wa binadamu na mawasiliano. Data zilizotumika katika makala hii zimepatikana katika machapisho ya kifasihi, hotuba na magazeti. Makala imeonyesha kuwa kiunganishi ‘na’ kina dhima mbalimbali za kipragmatiki ambazo ni uongezi, usababishi, ukinzani, usambamba na ufafanuzi. Dhima hizo ni fasiri ya mahusiano yaliyopo baina ya vishazi ambatani ambayo hayakusemwa kwa uwazi. Makala imeonyesha kuwa kiunganishi ‘na’ ni kiashiria muhimu cha kiisimu kinachomwongoza mshiriki wa mazungumzo kupata fasiri iliyokusudiwa kwa kudhibiti mchakato wa ufahamu. Pia, makala imeonyesha kwamba kiunganishi ‘na’ hutumika sambamba na viashiria vingine vya kiisimu na vya kiulimwengu kuashiria fasiri mahususi iliyokusudiwa baina ya vishazi vilivyoambatanishwa.